Kwa mujibu wa ripoti ya Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, katika siku za hivi karibuni, kufuatia uhalifu wa kigaidi unaojirudia wa utawala wa Kizayuni, Shahidi Haytham Ali Tabataaba’i (Abu Ali) alipata daraja ya shahada katika shambulizi la kikatili la utawala wa Kizayuni dhidi ya eneo la Haret Hreik katika viunga vya kusini mwa Beirut.
Shahidi huyu mtukufu, baada ya maisha marefu ya jihadi ya kweli, kwa ikhlasi, uaminifu na unyenyekevu, amejiunga na wenzake mashahidi.
Shahidi Haytham alikuwa mtu wa pili kwa cheo ndani ya Hizbullah ya Lebanon, na kuuawa kikatili kwa kiongozi huyu wa ngazi ya juu kumebeba ujumbe muhimu kutoka kwa adui wa Kizayuni kwenda kwenye Kambi ya Muqawama, hususani Hizbullah ya Lebanon.
Utawala wa Kizayuni katika kipindi cha usitishaji mapigano na Hizbullah ya Lebanon umevunja makubaliano hayo karibu mara elfu tano, na umesababisha mamia ya raia na wanajeshi wa Hizbullah ya Lebanon kuwa mashahidi.
Katika muktadha huo, mwandishi wa habari wa Hawza amefanya mazungumzo na Dkt. Hasan Al-Abbaadi, Mkurugenzi wa Kituo cha Tafiti cha Al-Mindhar: Al-Abbaadi, akirejea athari za kuuawa kwa Shahidi Haytham Tabataaba’i na malengo ya utawala wa Kizayuni katika jinai hii, amesema: Uchambuzi wa awali kuhusu kulengwa kwa Kamanda Shahidi Haytham Tabataaba’i unaonesha kuwa hili ni tukio la msingi katika mzozo kati ya Israel na Hizbullah, kwa kuwa kumlenga mtu wa pili kwa cheo na Mkuu wa Majeshi wa chama hiki kunaakisi ujumbe muhimu wa kimkakati unaozidi mbali ya kuondolewa kwa mtu na kiongozi mashuhuri pekee.
Akaendelea kusema: Mbali na tukio hili, kuna athari nyingi, kwa kuwa Hajji Haytham Tabataaba’i, maarufu kwa jina la “Abu Ali”, baada ya Sheikh Naim Qasim, alikuwa kamanda wa pili wa Hizbullah, na anahesabiwa kuwa ndiye kiongozi wa juu zaidi wa kijeshi kuuawa tangu makubaliano ya usitishaji mapigano mwishoni mwa mwaka 2024, ambapo shambulizi la Israel dhidi ya viunga vya kusini mwa Beirut lilipelekea kupata shahada kwake pamoja na wapiganaji wengine wanne wa Hizbullah.
Al-Abbaadi, akibainisha nafasi muhimu ya shahidi huyu katika Uwanja wa Muqawama wa Iraq katika mapambano dhidi ya magaidi wa kitakfiri na katika nyanja nyingine pia, amesema: Shahidi Haytham alikuwa na nafasi ya msingi katika kusimamia vita kwa ajili ya kuusaidia Muqawama wa Palestina huko Ghaza, na pia alikuwa na dhamana ya majukumu muhimu nchini Syria na Yemen.
Akiashiria ujumbe wa Israel kwa uongozi wa Hizbullah kupitia mauaji haya ya kinyama, amesema: Kupitia operesheni hii ya kikatili, Israel ilitaka kwa vitendo na pia kinadharia kufuta makubaliano ya usitishaji mapigano, na ionekanishe kushindwa kwake kama ni hatua ya nguvu, kwa kudai kuwa ina uwezo wa kuupiga moyo wa uongozi wa kijeshi wa Hizbullah.
Mkurugenzi wa Kituo cha Tafiti za Kimkakati cha Al-Mindhar amesema: Tunaamini kuwa hatua ya pili ya operesheni hii ni kudhoofisha uwezo wa Hizbullah na kuwalenga viongozi wake. Hata hivyo, msimamo wa Hizbullah unahesabiwa kuwa ni nguvu mara dufu, kwa kuwa uliandaa mazishi makubwa ya kitaifa kwa kamanda huyu shahidi na kumtaja kuwa ni “kiongozi mkubwa wa jihadi”.
Al-Abbaadi, akitaja sababu ya ukimya wa Hizbullah, amesema: Ukimya wa Hizbullah katika kipindi hiki ni dalili ya busara na hekima yake, na chaguo za kujibu zipo wazi mbele yao katika kila uwanja.
Katika hitimisho amesema: Mauaji haya yanaonesha uwezo wa chama hiki kulea viongozi wenye nguvu zaidi hata kuliko waliowatangulia. Adui Muisraeli huwaogopa wanazuoni na viongozi, kwa sababu wao ndio msingi na nguzo ya Muqawama.
Katika siku za karibu, Hizbullah kupitia mpango maalumu, thabiti na wa kimkakati, itaishangaza dunia.
Maoni yako